Ibrahim Kinana, wa CCM na Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youging |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshtaki Balozi wa China nchini, Dk.
Lu Youging kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kujihusisha na siasa katuika majukwaa
nchini kitendo ambacho ni hatari katika uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania
na China.
Pia kimemshtaki kwa Serikali ya China na ya Tanzania kikidai kitendo cha balozi
huyo ni kukiuka Mkataba wa Kidiplomasia wa Vienna (Vienna Convention of
Diplomatic Reletions of 1964 ibara ya 41 (1-3) ambao unasimamia sheria za nchi
wanachama w Umoja wa Mataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, Ezekiel Wenje alisema kitendo cha
Balozi wa China, Dk. Youging kujihusisha na siasa za uenezi katika Chama cha
Mapinduzi (CCM) ni kosa kubwa kimataifa na amepoteza sifa za kushikilia nafasi
hiyo.
Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) na Waziri Kivuli wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema balozi huyo amevunja sheria za Mkataba
wa Vienna ambao unasimamia sheria za nchi wanachama wa UN. Alisema kifungu alichovunja kinakataza
Balozi yeyote kujihusisha na shughuli nyingine ambazo haziendani na majukumu ya
uwakilishi wa nchi na nchi.
Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) Bw. Ezekiel Wenje
Wenje alisema balozi huyo anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kama
inavyoelekezwa katika mkataba wa Vienna kwamba ikiwa balozi atakiuka mkataba
huo atakosa sifa na ataondolewa kinga aliyonayo na kufikishwa kwenye vyombo vya
sheria.
Alisema: “Jambo hili katika macho ya diplomasia, limevunja misingi na taratibu
za ushirikiano wa kimataifa, wenye nia njema kwa wananchi wa pande mbili, baina
ya nchi na nchi na katika ngazi ya serikali.
“Kwanza ni taswira ya dharau ya hali ya juu ambayo Balozi wa China ameamua
kuwaonyesha Watanzania, hatuamini kwamba amepungukiwa na uwezo kiasi gani
lakini anapaswa kukumbushwa aweze kuheshimu mipaka ya majukumu na wajibu wa
diplomasia kwa nafsi ya balozi anapokuwa nchi ya ugenini.
“Balozi huyu anapaswa kukumbushwa kuwa uhusiano wa vyama, kwa maana ya Chama
cha Kikomunisti cha China na CCM hata kama ungekuwa mzuri kiasi gani hauna
mwingiliano na uhusiano wa Serikali ya Tanznaia na China.
“Hatutaki kuamini kuwa serikali ya China imemtuma Balozi Youquing kuja nchini
kufanya kazi za ukatibu mwenezi wa CCM, tumesikitishwa heshima aliyopewa na
Watu wa China ameidharau na amevuka mstari ambao hakuna mwanadiplomasia yeyote
makini anayeheshimu uhusiano baina ya nchi na nchi angejaribu kufanya hivyo.
“Mstari aliouvuka balozi huyu umefafanuliwa wazi katika Mkataba wa Vienna
Convention wa 1961 hasa katika kifungu cha 41(1) na 3, katika masuala
yanayohusu uhusiano na kinga za mabalozi, kwamba ni marufuku kwa
mwanadiplomasia yeyote kuingilia siasa za ndani za nchi mwenyeji wake.
“Chadema tunachukua hatua dhidi ya balozi huyo kujihusisha na chama cha siasa
kwa kuvaa kofia ya CCM na kuelezea mambo ambayo hayakupaswa kusemwa kwenye
majukwaa ya siasa.
“Kwanza tunaandika barua tatu, moja itakwenda Serikali ya China, ya pili
itakwenda UN na nyingine itakwenda Serikali ya CCM ambayo ndiyo imempeleka huko
mikoani.
“Barua hizo zitakuwa zinataka kueleza msimamo wa tukio hilo la balozi wa China
nchini kujihusisha na siasa za majukwaani na kuvaa nguo za CCM, tunataka kujua
hatua gani zitakazochukuliwa haraka kabla ya Chadema hatujapendekeza hatua za
kuchukua.
“Hii ni hatari kwa balozi huyo kujiingiza kwenye siasa kitendo kinachosababisha
kuhatarisha uhusiano uliopo kati ya wawekezaji wa China nchini kwa sababu
wananchi wanaweza kutafsiri vibaya.
“Kwa mfano kuna maeneo ni ngome za Chadema na pale kuna wawekezaji wa China
wanaweza kukataa kutoa ushirikiano wakidai ni wapo mlengwa wa CCM, pia ni
hatari chama kingine kitapokuja kushika dola hakutakuwa na uhusiano mzuri.
“Tutaambatanisha ushahidi wa kutosha katika barua hizo ikiwa ni pamoja na picha
za mnato na video, maneno aliyotamka kwenye mkutano, picha inayoonyesha akiwa
amveaa sare za CCM na jinsi anavyocheza”.
Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youging akiwa katika mikutano ya CCM
Picha zilizonyeshwa kwa waandishi wa habari zilionyesha Balozi Youging akiwa
katika mikutano mbalimbali ya CCM maeneo ya Kishapu, Shinyanga na Kahama. Katika
picha hizo balozi huyo alionekana amevaa sare za CCM, akihutubia na kuendesha
baiskeli akiwa na viongozi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Abdulrahman
Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. Kwa mara ya kwanza balozi
huyo aliibukia katika mkutano waCCM uliofanyika Shinyanga huku akishangiliwa na
wananchi alipojaribu kuzungumza kisukuma.
CCM yazungumza
Wakati huohuo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimesikitishwa na hatua ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumshutumu Balozi wa China, Dk. Lu Youqing kwa kuhudhuria mikutano ya CCM. Kimewataka watanzania kupuuza madai
ya Chadema kikisema hayana msingi kwa maendeleo ya taifa na watu wake.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alikuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha
Mwandoya wilayani Meatu.
Nape Nnauye - Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi
Alisema ni wazi Chadema kinataka kutumia matatizo ya wananchi kuyageuza agenda
ya siasa.Chadema haina budi itambue kuwa chama tawala cha China (CPC) kimekuwa
na urafiki wa muda mrefu na CCM ikizingatia Balozi Dk. Lu pia ni kiongozi wa
chama hicho. Nape alisema hatua ya Balozi huyo kuhudhuria mkutano huo ni
mafanikio ya ziara ya iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
China mapema mwaka huu.
“Balozi Dk. Lu amekuja kuleta ukombozi kwa watanzania hasa wa Kanda ya Ziwa kwa
kuleta wawekezaji katika Mkoa wa Shinyanga kwa kujenga viwanda wa nyuzi, pamba,
nyama, maji na ngozi ambako ajira zaidi ya 1000 zitapatikana.
“Watanzania wapuuze madai haya kwani si dhambi kwa Balozi wa China kuhudhuria
mkutano wa CCM… urafiki wetu hakuanza leo ni wa muda mrefu katika historia ya
nchi hizi mbili tangu na baada ya Uhuru,” alisema Nape. Nape alisema CCM
imepitaka kila eneo la yakiwamo majimbo yanayoongozwa na wapinzani na kubaini
kuwapo changamoto nyingi.
Aliitaka Chadema kwenda kutatua haraka matatizo hayo badala ya kufanya mikutano
Dar es Salaam pekee. Wiki iliyopita akiwa mjini Shinyanga Balozi Dk. Lu
Youqing, alihudhuria mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kuwa
hakuna chama imara kama hicho.
No comments:
Post a Comment