Wise AD

Wise AD

Saturday, December 22, 2012

‘Wananchi Dar hawawajui wabunge wao’



Mkurugenzi wa  taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza,  Rakesh Rajani akielezea juu ya utafiti walioufanya kuhusu  Huduma, Sera na viongozi  walioko madarakani kwa mwaka huu jijini Dar es Salaam jana, Kulia ni mtafiti wa taasisi hiyo.


UTAFITI mpya uliotolewa na Taasisi ya Twaweza, umeonyesha kuwa wakazi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawaridhishwi na namna Serikali inavyoshughulikia utoaji wa huduma za msingi huku nusu yao ikiwa haiwajui wabunge wao wala hawajawahi kuwaona.
Majina ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam na majimbo yao katika mabano ni Idd Azan (Kinondoni), Zuberi Mtemvu (Temeke), Dk Makongoro Mahanga (Segerea), Musa Zungu (Ilala), Faustine Ndungulile (Kigamboni), Eugene Mwaiposa (Ukonga), John Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe).
Utafiti huo uliofanyika Agosti hadi Septemba mwaka 2010, ulihusu Mkoa wa Dar es Salaam, wanachukuliaje suala la utawala na maoni ya watu kuhusu huduma, sera na viongozi.
Akitangaza matokeo ya utafiti huo, jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajan, alisema wabunge huchaguliwa katika majimbo na wananchi.
Alisema wananchi wanapaswa kujua namna ya kufikisha malalamiko na mawazo yao kwa wabunge wao kuhusu huduma za msingi zinazotolewa na Serikali.
Alisema ni jambo la kushangaza kwamba asilimia 46 ya wakazi wa Dar es Salaam waliohojiwa, hawajui hata jina la mbunge wao wala kumwona.
Alisema utafiti huo ulihusisha Wilaya za Kinondoni, Ilala, na Temeke na kwamba ulizihusisha kaya 550.
Katika utafiti huo, waliohojiwa hawakuulizwa kwa nini hawamfahamu mbunge wao licha ya asilimia 94 kuwa na kitambulisho cha mpigakura ikionyesha kwamba walijiandikisha kupiga kura.
Rakesh alisema kati ya waliohojiwa, zaidi ya asilimia 75 hawaridhishwi na namna huduma za huduma za kijami zinavyotolewa huku huduma za majisafi na salama, zikiwa hazishughulikiwi ipasavyo.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, wananchi walionyesha kuwa na imani zaidi kwa polisi na mahakama katika utendaji wa kazi kuliko Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Majisafi na Majitaka (Dawasco).
Utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia 65 ya waliohojiwa wanaiamini mahakama, asilimia 62 wanaiamini polisi huku asilimia 29 wakiwa na imani na Dawasco na asilimia 43 wakiiamini Tanesco.
“Wakazi wa Dar es Salaam hawaoni  kama Dawasco na Tanesco zinatekeleza shughuli zao kwa manufaa ya wananchi,” alisema Rakeshi akinukuu sehemu ya matokeo ya utafiti.
Kuhusu rushwa, utafiti huo umeonyesha kwamba licha ya wananchi kuwa na imani na polisi na mahakama, asilimia 60 ya wananchi waliohojiwa walisema rushwa imeongezeka nchini kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
Karibu asilimia 29 ya waliohojiwa, walisema katika kipindi cha miezi 12 iliyopita, walijikuta wakilazimika kutoa rushwa ili wapate huduma katika vituo vya afya ambako huduma hizo hutolewa bure. Utafiti huo ulionyesha kwamba zaidi ya mtu mmoja kati ya wahojiwa 10 walisema walitoa rushwa kwa polisi ili kuepuka kutozwa faini au kupata adhabu nyingine. Utafiti huo ulionyesha kwamba viongozi wa dini ndiyo wanaoaminiwa zaidi kufanya kazi kwa masilahi ya wananchi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wananchi waliulizwa ni kwa kiasi gani wana imani na aina mbalimbali za viongozi ambao wanafanya kazi kwa masilahi ya wananchi na siyo kwa maslahi yao binafsi.

No comments:

Post a Comment