Hivi karibuni bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha muswada wa sheria ya fedha
iliyosainiwa na rais Jakaya Kikwete na kuanza kutumika kama sheria kuanzia tarehe
01 August 2013. Sheria hii imetaja chanzo kimojawapo cha mapato kama tozo ya
shilingi 1,000 kwa kila laini ya simu (sim card).
Kama mwitikio wa sheria hii,
wananchi wengi kwenye mitandao ya kijamii waliipinga tozo hii na kwa kupitia
jukwaa la Change Tanzania, kuanzia tarehe 15 Julai 2013, juhudi zilianza za
kukusanya maoni ya wananchi kwa njia mbili: kwa njia ya mtandao – online
petition – na kwa njia ya kukusanya sahihi za wananchi mitaani.
Hadi kufikia tarehe 13 August
2013, Change Tanzania kwa njia hizi mbili imekusanya zaidi ya sahihi elfu nne
(4,000) kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara,
Mwanza, Shinyanga, Singida, Songea, Zanzibar na mikoa mingine. Juhudi bado zinaendelea
za kukusanya sahihi zaidi.
Wito wa kusitisha tozo/kodi
hii imeainisha kwa kina ni kwanini wananchi wanaipinga ikiwa ni pamoja na kuwa
kodi hii ya laini ya simu inamkandamiza mtanzania wa
hali ya kawaida na wa hali ya chini ambao ni 67% ya wananchi wanaoishi chini ya
kipato cha dola 1.25 (shs 2,000) kwa
siku. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wamiliki wa laini za simu milioni 22,
milioni 8 wanatumia chini ya shilingi 1,000 kwa mwezi.
Wito huu umeeleza kuwa kuwaongezea
mzigo wananchi hawa kwa kiwango ambacho tayari wanashindwa kumudu ni kuwanyima
kabisa fursa ya kutumia huduma hii muhimu. Sababu nyingine iliyotajwa kwenye
wito huu ni kuwa kodi hii haifuati misingi ya kulipa kwa kadri ya matumizi na
ni kodi kandamizi inayotozwa kwa wamiliki wa laini za simu wote kwa kiasi
kimoja bila kuzingatia kiwango cha matumizi.
Wito huu unasisitiza kuwa hii
inamkandamiza mwananchi wa hali ya chini kwa kumlazimisha kulipa kiwango
kikubwa cha kodi ikiwa ni tofauti na mapato yake. Mfano uliotolewa kwenye wito
huu ni wa mtu anayetumia shilingi laki tano kwa mwezi kama muda wa maongezi na
yule anayetumia shilingi elfu tano - na tukilinganisha uwiano wa malipo haya na
matumizi yao – basi yule anayetumia shilingi laki tano analipa 0.2% ya matumizi
yake, ila yule anayetumia shilingi elfu tano anatozwa 20% ya matumizi yake.
Aidha wito huu pia umeainisha sababu nyingine ya kiuchumi kwani tayari kodi
nyingi zimeongezwa kwenye sekta hii ya mawasiliano.
Wito huu umesisitiza kuwa
kodi hii
ni juu ya ongezeko la kodi mbalimbali katika huduma za simu za mkononi ikiwa ni
pamoja na kuongezeka kwa ushuru kutoka 12% kwenda 14.5% na pia kodi hii kutozwa
kwa huduma zote ingawa awali ilitozwa kwa huduma ya matumizi ya kuongea. Wito
huu unainisha kuwa hivi sasa utumiaji wa internet, kutuma na kupokea pesa kwa
njia ya simu za mkononi unatozwa kodi, hivyo ongezeko hili pekee limeshafanya
huduma za simu za mkononi kupanda gharama kwa kiasi kikubwa, na ongezeko la tozo/kodi
ya shs 1,000 litazidi kuwaumiza wananchi.
Wito
huu pia umependekeza kuwa mapato ya ndani yanaweza kupatikana kupitia njia
zingine mbadala ikiwa ni pamoja na serikali kupunguza matumizi yake mengineyo (safari, posho, semina,
manunuzi ya magari na kudhibiti ufisadi) na imetaja utafiti uliofanywa na Interfaith Standing Committee on Economic
Justice and the Integrity of Creation mwaka
jana uligundua kuwa kwa wastani Tanzania hupoteza dollar za kimarekani billion
moja (takriban shs trilioni 1.8) kila mwaka kutokana na ukwepaji kodi,
uhamishaji haramu wa fedha na misamaha ya kodi.
http://www.avaaz.org/en/petition/WITO_WA_KUSITISHA_TOZOKODI_YA_LAINI_YA_SIMU_KILA_MWEZI_KUFUATIA_MABADILIKO_YA_SHERIA_YA_KODI_2013/
Change Tanzania ilianza mwaka
2012 kama mwamko wa wananchi waliopo katika mtandao yaani social networks kwa
maana ya Twitter na Facebook, kutaka
kujadili masuala yanayohusu nchi yetu kama wananchi bila itikadi ya kisiasa na
kwa kuzingatia umuhimu wa kuwajibisha viongozi wa ngazi zote na hivyo kuleta
mabadaliko chanya katika jamii yetu kwa njia ya mijadala. Baada ya kupata
wanachama zaidi ya elfu 20 (20,000) ndani ya mwezi moja, baadhi ya waanzilishi
wa kikundi hiki cha mtandao waliisajili kama kampuni isiyo na hisa yaani
isiyotengeneza faida (not for profit company).
Leo hii ChangeTanzania ina
wanachama zaidi ya elfu 30 Facebook, na wafuasi zaidi ya elfu 6 (6,000)
Twitter. Pia tuna blog na ukurasa wetu wa internet (website) www.changetanzania.org.
Change Tanzania haipokei
msaada wowote wa kifedha au udhamini kutoka mashirika mengine, vyama au taasisi
bali hutegemea michango ya wanachama wake tu.
Maria Sarungi Tsehai
MRATIBU
Simu: +255 783 034403
Barua pepe:
sarungim@gmail.com
No comments:
Post a Comment